Home  |  Search  |  Help  |  Contact Us  |  Rutgers University Swahili


Practice
101 Assignments
101 Exercises
102 Assignments
102 Exercises
201 Exercises
202 Exercises
Discussion


Somo la nne: Kujipatia Mchumba

Sources: Source: Kujipatia Mchumba. Dar es Salaam: Jumuiya ya Kikristo Tanzania, 1981, pp. 28-29.

Nafanya kazi ofisini. Mchumba wangu ana-taka niache kazi nikae nyumbani. Ameahidi kunipa kila mwezi mara mbili ya mshahara wangu wa sasa. Nampenda kufa, na ningetaka niolewe1 naye. Nifanye nini?

Ijapokuwa unampenda kufa lakini huna budi2 umwulize au ujiulize mwenyewe maswali machache. Je, ni kwa nini hataki uendelee kufanya kazi? Je, anatazamia kukuoa lini? Je, uchumba wenu ukivunjika itakuwaje?3 Je, akifungwa, au akiugua, au donge analopata likitoweka wewe utakuwa wapi? Je, maisha ya kuzurura nyumbani bila kazi ni kitendo cha maendeleo?

Ni dhahiri kuna kitu huyu mchumba anacho-kiogopa ikiwa4 utazidi kuendelea5 na kazi yako huko ofisini. Pengine ana wivu6 kwamba huko ofisini una wapenzi wengine. Pengine anahofia kwamba utakutana na7 wengine huko ambao watakunyakua. Kwa vyovyote8 huyu mchumba hafikirii maslahi yako bali yake mwenyewe. Ikiwa ameanza kukufuga na kukupa masharti hivi mapema kwenyeuchumba, je akishakuoa unatazamia uhuru wa aina gani? Maoni yetu ni kwamba mchumba huyu hakufai. Achana9 naye.

Niko masomoni bado, mchumba wangu ambaye nampenda sana anataka tuoane mapema. Je, niache masomo au nimwache yeye?

Kama upo uwezekano10 wa kuendelea na masomo yako baada ya kuoana hakuna sababu yo yote ya kumwacha. Vilevile kama unao uhakika kwamba maisha yenu katika ndoa yatakuwa mazuri ni afadhali usikubali kumpoteza. Lakini si vizuri ukatishe masomo yako kwa kumkimbilia mchumba ambaye huna hakika ya maisha yako naye baadaye. Kwa kuwa masomo yako yatakuwa na faida11 kwenu wawili na pia kwa jamaa na nchi nzima, itafaa12 umtafadhalishe mchumba wako akusubiri mpaka umalize masomo.

Ikiwa kweli naye anakupenda bila shaka atakubali. Akikataa, na ukiona kwamba hana sababu kubwa ya kutaka mwoane mapema, basi unaweza kukataa kukatisha masomo yako. Hapo itakuwa hiari yake kukungojea ama kutafuta mchumba mwingine. Mara nyingi wachumba wanaotaka kuvunjia wenzao13 masomo huwa ni14 wale wenye wasiwasi kwamba huenda wakapigwa teke15 hapo baadaye.

MASWALI

1. Mwandishi wa kwanza ni mwanamke au mwanamume? Unajuaje?

2. Kama mwandishi wa kwanza akikubali kukaa nyumbani, mchumba wake amesema kwamba atafanyaje?

3. Waandishi wa barua hizi ni wafanya kazi au sivyo?

4. Mwandishi wa pili ana shida gani?

5. Je, Majibu katika somo ni kama yale ambayo wazazi au ndugu wangetoa? Au ni kama majibu ya watu ambao hawajakutana na wanaouliza? Unajuaje?

6. Eleza kwa ufupi namna za woga ambazo wachumba wengine wanazo.

7. Maandishi kama hayo kwa kawaida hupatikana wapi? Toa mfano mmoja wa maandishi mengine ya aina hii.

8. Anayejibu anasema ni afadhali mwandishi wa pili afanyeje?

9. Rafiki yako akikuuliza maswali kama yaliyomo katika somo, utajibuje? Eleza kwa ufupi.

-----------------------------------------------------------------

MSAMIATI

mchumba/wachumba - kijana aliyeposa au aliyeposwa

kuahidi - mtu kusema kwamba bila shaka atafanya kitu fulani

kupenda kufa - kupenda sana

anatazamia kukuoa lini - anafikiri kukuoa lini

uchumba - hali ya kuwa na mpango wa kuoana

kufungwa - kukamatwa na polisi na kuwekwa mahali mbali ya wengine kwa sababu ya kukosa

kuugua - kupata ugonjwa

donge analopata likitoweka - kama hatakuwa na mshahara

kuzurura nyumbani - kuweko nyumbani tu, bila kitu cha maana cha kufanya

kitendo cha maendeleo/vitendo vya maendeleo - jambo linalofanya maisha yawe bora

ni dhahiri - ni rahisi kuona au kufahamu

kuogopa - kuwa na woga

kuwa na wivu - kufikiri pengine mpenzi wako ana wapenzi wengine

kuhofia - kuogopa

kukutana na - kuonana na mtu fulani kwa mara ya kwanza

kunyakua - kuchukua

maslahi – faida

uwezekano – njia ya kuweza, hali ya kuwezekana

uhakika – hali ya kutokuwa na shaka

kupoteza – kukosa kukiona (kitu)

kukatisha masomo yako – kuacha kusoma

kukimbilia – kumfuata mtu bila kutumia akili

kutafadhalisha – kusema “tafadhali”

kusubiri – kungoja

kufuga - kuweka, mtu, mnyama au ndege nyumbani ili asitoke

kupa masharti – kulazimisha kufanya kitu

maoni – mawazo

kufaa – kuwa na faida

kuachana na – kutoendelea na (mpenzi)

hiari – kuchagua

kuvunja - kufanya kitu kivunjike

wasiwasi - woga


[kifungu hiki kimenakiliwa kutoka kitabu Masomo ya Kisasa na Ann Biersteker et al.]



Reference
362
Grammar
Vocabulary

Special Characters
Instructors Notes


© 2002 Rutgers University, excluding excerpted material that remains under the ownership of the existing copyright holders.

digiclass_help@brokenmail.rutgers.edu please replace "brokenmail" with ctaar.rutgers.edu