Home  |  Search  |  Help  |  Contact Us  |  Rutgers University Swahili


Practice
101 Assignments
101 Exercises
102 Assignments
102 Exercises
201 Exercises
202 Exercises
Discussion
 1                                 

Kiswahili ni lugha ambayo inazidi kuwa muhimu katika Jamhuri ya Kenya.

Wakati wa utawala wa Mwingereza, kilikuwa kikitumika kwa kuwa watawala hao walikiona kina faida ijapokuwa upande mwengine kilikuwa pingamizi katika kuwateka akili wenyeji wa nchi hizi. Basi kilikuwa ni kiovu ambacho walikuwa hawana budi kuwa nacho. Ndipo kisitupwe kabisa. Kilikuwa kikifundishwa katika shule za Kiafrika na watumishi wa Serikali walikuwa wakitarajiwa kukijua. Wanafunzi walifanyiwa mtihani wa Kiswahili katika daraja mbalimbali za masomo yao na watumishi wa Serikali walitarajiwa kufikilia viwango maalumu katika ujuzi wa lugha hii. Bila ya hivyo nyongeza za mishahara yao zilikuwa zikizuiwa mpaka wafike kima kilichotakiwa.

Tangu baada ya kupatikana uhuru shule za waalimu, za sekondari na za aina nyingine pia zinazidi kukiendeleza Kiswahili. Katika Chuo Kikuu cha Nairobi vile vile Kiswahili kinafanyiwa hima kubwa siku hizi na watumishi wa Serikali wapelekwao kujifunza katiba za utawala na maendeleo, wanapata mafunzo maalumu ya Kiswahili.

Kila uchao zile fikira tulizokuwa tukijazwa —ati Kiswahili ni lugha ya kigeni, lugha pungufu, na kadhalika — zinazidi kufichuliwa kuwa ni fikira za kutuziba macho tu kukitweza Kiswahili. Watu wanazidi kufunukiwa kuwa lugha hii ni ya kienyeji, ni ya kale na ina ukwasi wa fikira na matumizi kama lugha nyingine zozote kubwa za ulimwengu. Kwa hivyo Kiswahili kinazidi kuungwa mkono na kutiliwa nguvu na hapana shaka baada ya muda si mrefu Kiswahili kitakuwa lugha rasmi ya taifa katika Jamhuri ya Kenya kama kilivyo katika Jamhuri ya Mwungano wa Tanzania, na wakati huo kitasomeshwa skuli zote.

 

A

1   Mwandishi anatuonyesha kuwa watawala waliopita:

a) walifanya kusudi kutufunza tuidharau lugha yetu.

b) walituonyesha kwa moyo safi kuwa lugha yetu ni pungufu.

 

2  Chagua neno lililo sawa, katika maneno uliyopewa katika vifungo, kukamilisha kila sentensi:                     

(i)    Watawala wa........ walikiona Kiswahili kina faida (Kenya; Kiingereza)

(ii)   Kiswahili ..... katika shule zilizokuwa za Kiafrika (kikifundishwa; hakifundishwi)

(iii)   Watumishi wa Serikali ……. kufanya mitihani ya Kiswahili (walilazimishwa; waliombwa)

(iv)   Nyongeza za mishahara ……. mpaka mtumishi wa Serikali apasi mtihani wa Kiswahili (zilikawilishwa; zililipwa)

(v)    Baada ya uhuru lugha ya Kiingereza Kenya ........ kuwa muhimu  (ilipungua; iliendelea)

(vi)   Katika maskuli mbalimbali Kiswahili kinazidi ……. (kuendelezwa; kupunguzwa).

 (vii) Kiswahili kinafundishwa katika shule........ za sekondari (nyingi; zote).

(viii) Katika Chuo cha........ cha Kenya mafunzo maalnmu ya Kiswahili yanatolewa (Utawala; Taarifa).

 

B

3  Eleza maana ya:

(i)    kuwateka akili

(ii)   viwango

(iii)   fanyiwa hima

(iv)   tweza

(v)    kufichuliwa

 

 

C

4.    Wale wasemao kuwa Kiswahili ni lugha ya kigeni, hutoa ushahidi gani, na wale wasemao kuwa si lugha ya kigeni hutoa sababu gani?

 

4.    Darasa lijadiliane kuhusu haabari ifuatayo: Kiswahili ni lugha ambayo yafaa sana kuwa lugha ya taifa katika nchi yetu (yn., ya Kenya)

 

 

 

Kusoma na Kufahamu Kiswahili, IV; 1-3]

 

(Imerekebishwa kidogo tu.)

 

 



Reference
362
Grammar
Vocabulary

Special Characters
Instructors Notes


© 2002 Rutgers University, excluding excerpted material that remains under the ownership of the existing copyright holders.

digiclass_help@brokenmail.rutgers.edu please replace "brokenmail" with ctaar.rutgers.edu