|
2 8 Kiswahili cha Karne Hii Kutoka: Jarida la Chuo cha Uchunguzi ua Lugha ya Kisuahili, No. 28/1, uk. 33-36. Muandishi: Salehe Kibwana wa Tanga. Bwana Salehe Kibwana katika hotuba yake aeleza kwa kifupi mabadiliko machache yaliyotokea katika lugha hii. Toka habari hii iandikwe, yame-tokea mabadiliko zaidi ambayo itafaa vile vile kuyajadili. Asalaam Aleikum naishukuru sana Jumuiya ya Taaluma ya Kiswahili kwa kunifanya niwe mmoja wa watu waliochaguliwa kuhutubu katika ukumbi huu, habari maalumu juu ya lugha yetu nzuri hii ya Kiswahili. Kusema kweli mimi ni mwoga mno wa kuchukua heshima kubwa kama hii, kwani pengine hufikiri si stahili yangu, sababu mimi si mtaalam wa mambo kama haya, na kisha sikujizoweza kutoa hotuba mbele ya watu wengi namna hii. Lakini basi sikuweza kuwatia tope za uso wale walionipa heshima hii kwani wahenga walisema: Uitwapo itika, ushikwapo shikamana, likichwa lala, fungu la masikini haliondoki. Natumaini kila mtu hapa methali hii inamwelea vizuri. Basi kisa hivyo nimeitikia wito huu na kuipokea heshima hii kwa mikono miwili. Kwa faida ya wale ambao ndio mara ya kwanza leo kuhudhuria hapa, nawafahamisha kuwa hii sasa ni mara ya nne kutolewa hotuba za namna hii hapa Tangamano katika mwaka huu. Mara ya kwanza alihutubu bwana Hakimu Juma Mwindadi, juu ya Ubora wa Kiswahili katika lugha za dunia. Mara ya pili bwana Mohamed Ali alihutubu juu ya Kiswahili toka ngambo hata ngambo. Na mara ya tatu bwana Dowsett D.C. wa Tanga nje alieleza historia ya nchi hizi za Afrika ya Mashariki kuanzia miaka elfu tatu iliyopita mpaka leo. Mara ya nne ni hii leo yangu mimi ambaye nimetakiwa nizungumze juu ya Kiswahili cha karne hii. Kama ijulikanavyo na kila mtu, karne ni muda wa miaka mia moja. Basi ikiwa ni hivyo, ni wazi kwamba natakiwa nizungumze juu ya Kiswahili kilichoanzia toka mwaka 1901 na ambacho kitaendelea mpaka mwaka elfu mbili (2000) tukijaliwa. Hakika Kiswahili tangu mwaka 1901 kimekutana na misukosuko mingi sana; kwani tangu wakati huo nilioutaja nchi yetu imepata maendeleo mengi ambayo yameletwa na wageni; kama vile biashara, mambo ya starehe, na utaratibu wa Serkali. Mambo haya matatu ambayo ni ya muhimu sana katika kila nchi ndio yanayofanya lugha yoyote ya wenyeji ionekane kuwa haitoshi. Ebu tuanzie kwenyi biashara. Mnunuzi aliyechukua vitu kwa mkopo, baadaye hupelekewa karatasi ya hisabu iitwayo bill. Mwendo huu wa kuchukua mali za watu kwa mkopo umekuja na wageni; kwa hivyo hatuna neno maalum la tafsiri ya Bill isipokuwa kwa maelezo. Kama ungemwambia mwenye duka 'kesho nipate karatasi ya hesabu yangu' mtu mwingine aweza kudhani kuwa labda umeweka amana yako ya fedha pale dukani, na sasa unataka uletewe hesabu ili ujue zimefika Shillings ngapi, kumbe hali unayedaiwa ni wewe. Mfano mwingine ni kama mahali pa kufanyia kazi za Maandishi; daima hujulikana kwa jina la 'Ofisi.' Basi kama ungetaka kutumia jina la Kiswahili ingekupasa kutumia maneno matatu, yaani 'chumba cha kuandikia' ndipo mtu mwingine angeweza kuelewa kwamba unataka kutaja Ofisi. Na kwa upande wa mambo ya starehe, ile hitilafu iliyoko baina yetu na wageni katika michezo, mambo ya utabibu na mengineyo, ndiyo inayofanya tutumie maneno ya kigeni ili kupata maana kamili ya neno tulitakalo. Kwa mfano ni rahisi mtu kufahamu ukisema ninakwenda welfeya kuliko ungesema 'Ninakwenda katika Jumba la Starehe au Jumba la Michezo,' sababu Welfeya sio mahali peke yake penye michezo katika mji wowote. Nawapa pongezi mabingwa walioyapatia majina maalumu majumba haya ya Welfeya, kama vile Tononoka kule Mombasa. Raha ya Leo huko Unguja na Tangamano hapa kwetu. Kadhalika kama ukisema 'nimenunua radio' mtu hawezi kutatizika, kuliko ungesema, 'Nimenunua simu ya upepo', sababu kuna chombo kingine maalumu cha kupokea na kupelekea simu kiitwacho ‘wireless' hiyo hasa ndio simu ya upepo. Vilevile mtu atatahamu upesi kama ukimwambia 'Nimekula kwinini' kuliko ukisema mmekula ‘dawa ya homa’, sababu ziko dawa za namna nyingi kwa maradhi ya homa. Hivyo inaonyesha dhahiri kwamba tukitaka tusitake mara nyingine ni lazima tutumie maneno ya wageni kufupisha maelezo mengi kwa mambo na vitu walivyokuja navyo wao. Mfano kama ‘motokari’, kwa Kiswahili jina lake lingekuwa gari linaloendeshwa na moto barabarani lenye miguu mine. Unaona basi kama tungetumia maneno manane badala ya moja, na hivyo tungekuwa tunatumia wakati mwingi zaidi kwa mazungumzo machache tu. Juu ya serikali nayo, kuna mambo mengi mno yaliyoletwa na wageni. Lakini kwa vile sisi pia tulikuwa na utawala wetu hapo kale, imekuwa rahisi kidogo kuyapata maneno mengi yanayohusu mambo ya Serikali na ni machache tu yaliyo-tupungikia. Katika jumla ya maneno yaliyo na upungufu katika Kiswahili nitataja machache tu, katika mambo ya Serikali. Tuseme 'Gavana', Ni kweli kwamba tafsiri ya Gavana ni liwali kwa Kiswahili, lakini haiwezi kuleta maana halisi kama tungetaja bwana Gavana wa Tanganyika kwa jina la liwali, sababu yuko Liwali Dar es Salaam, Liwali Tabora na penginepo. Au D.C. ukisema Bwana Shauri itatatiza watu, sababu wapo wanaofanya kazi chini ya Bwana D.C. ambao hujulikana kwa jina la Mabwana Shauri. Na ukimwita Bwana Shauri mkuu watu wengi watadhani kuwa ni Bwana Hakimu Mkuu yaani Jaji Kata. Hapa nimetaja mifano ya maneno machache tu ambayo yameshambulia Kiswahili kwa sababu za halali kabisa. Sababu majina haya mliyoyataja na mengi mengineyo yana walakini katika Kiswahili. Na mtu kujaribu kutia ufundi wowote kutia neno la Kiswahili badala yake ni kuharibu lugha. Ni kweli kutumia neno la kigeni kunaweza kusemwa ni kuharibu lugha iwapo neno hilo laweza kupatikana katika lugha yenyewe. Kwa mfano hakuna sababu kusema nipe glass mahali pa nipe bilauri. Au fulani yuko 'remand' mahali pa fulani yuko mahabusi au amekata 'appeal' mahali pa amekata rufani. Au nakwenda 'customs' mahali pa nakwenda Forodhani. 'Family' yangu, mahali pa Jamaa yangu au Watoto wangu. 'Market', mahali pa Sokoni. 'Beach', mahali pa ufukoni na kadhalika. Kwa yote haya niliyotaja inaonyesha wazi kwamba Kiswahili cha karne hii sio sawa na kile cha karne iliyopita, hiki cha karne hii kimeongezeka sana, na kitazidi kuongezeka, kwa kadri ya mambo ya ulimwengu yanavyoendelea. Ni jambo la kufurahisha kuona kwamba Waswahili wa karne hii wanajitahidi kufanya mipango ya kuhifadhi Kiswahili kisiharibike, na baadhi ya Waswahili hao ni hawa wenye Jumuiya hii ya Taaluma ya Kiswahili, ambayo imetukutanisha sisi hapa leo kusaidiana nao. Namaliza hotuba yangu kwa kuwashukuru nyote mliovunja shughuli zenu za maana na kuhudhuria hapa kusikiliza maneno yangu. Ahsante sana. Jibu maswali yafuatayo:
1. Mwandishi asema ni mambo gani matatu ambayo ni jaribio kubwa la utoshelezi wa lugha ye yote?
2. Kwa nini mwandishi asema 'tukitaka tusitake mara nyingine ni lazima tutumie maneno ya kigeni?' 3. Maneno “Simu ya Upepo” yana maana nyingi katika Kiswahili. Itafaa kujadiliana juu ya maneno ya Kiswahili na ya Kiingereza ya namna hiyo, kisha itaafaa kutazama jinsi hali hii inavyoweza kuleta matatizo katika kazi ya kutafsiri. 4. Mwandishi atuambia nini kuhusu Kiswahili cha karne hii kikilinganishwa na kile cha karne iliyopita?
5. Kiswahili cha Bi Morningstar ni cha karne hii au cha karne iliyopita? [kutoka kitabu MAENDELEO YA KISWAHILI NA MAZOEZI: Makusanyo ya Maandishi na George A. Mhina] (imerekebishwa kidogo)
|