Home  |  Search  |  Help  |  Contact Us  |  Rutgers University Swahili


Practice
101 Assignments
101 Exercises
102 Assignments
102 Exercises
201 Exercises
202 Exercises
Discussion
 

ASILI YA KABILA NA UTARATIBU WA JAMAA

 

Utaratibu wa kabila la Gikuyu wategemea mambo matatu makubwa, ambayo bila kuwako hakuwezi kuwa na umoja katika shughuli za kabila. Kwani tabia na hali ya kila mtu katika kabila la Gikuyu hudhihirishwa na kanuni tatu kuu ambazo tutazieleza hapa kila moja.

     Ya kwanza ni ujamaa (mbari au nyumba) ambayo huunganisha watu wote wenye udugu wa damu; yaani mwanamume, mkewe au wake zake na watoto na pia wajukuu wao, vitukuu na vilembwe.

     Ya pili ni ukoo (muhiriga) unaounga katika kundi moja vikundi vidogo vidogo vya mbari ambavyo jina la ukoo wao ni moja na wanasadikiwa walitoka kwa jamaa moja zamani za kale. Ni wazi kwamba kwa ajili ya desturi ya kuoa wanawake wengi, jamaa moja au mbari huongezeka haraka, na katika kizazi kimoja inawezekana mbari hiyo kuwa na watu mia moja au zaidi. Kwa hivyo mnamo vizazi vichache idadi hiyo huongezeka kuwa maelfu kadha, na hapo huwa shida kwa mbari hiyo kuishi pamoja kama kundi moja ambako wangeitana baba, mama, dada, ndugu, mjomba, shangazi, babu, nyanya na kadhalika.

     Vitambulisho hivi vya udugu wa damu vikitoweka, kiungo cha pekee kinachobaki katika kundi ambalo hapo zamani lilikuwa limeunganishwa na uhusiano wa damu ya karibu karibu, ni muhiriga tu. Muhiriga hufunga-manisha pamoja jamaa wasiokaribiana na hii huwafanya wafikirie kusaidia-na katika mambo yote muhimu kwa manufaa na starehe ya muhiriga. Ili wazo hili lisisahauliwe, watu wa muhiriga mmoja hukutanika kwa kawaida wakati wa sherehe kubwa kubwa, vile kama arusi na tohara. Katika sherehe hizo wazee wa kila mbari humleta kijana mmoja. Vijana hawa huletwa pamoja wakajulishwa kila mmoja kwa mwenzake na kuelezwa vile ukoo wao unavyounga mbari yao kwa muhiriga. Vijana hao huelezwa mambo haya ili kwamba wakiwa watu wazima na kuchukua madaraka katika uongozi wa mbari zao, waweze kuendesha kwa busara shughuli za jamaa zao, na kadhalika wafuate mwenendo mzuri kama babu zao katika kukuza umoja wa muhiriga mzima.

     Kanuni ya tatu kubwa katika kufanya Gikuyu kuwa kitu |kimoja ni desturi ya hirimu (riika). Kama tulivyoona, utaratibu wa mbari na muhiriga husaidia kuunda makundi ya jamaa ndani ya kabila; kila kikundi kikiendesha shughuli zake peke yake lakini utaratibu wa mariika huunganisha na kuimarisha kabila zima katika shughuli zake zote.

     Karibu kila mwaka, maelfu ya wavulana na wasichana wa Gikuyu hutimiza ibada ya tohara, na bila masharti mengine wakawa katika kundi la hirimu moja (riika rimwe), bila kujali mbari, muhiriga au wilaya ya kila mtu. Watu hafanya shughuli zao pamoja kusaidia kabila nao huwa kama ndugu na dada. Hivyo, katika kila kizazi utaratibu wa kabila la Gikuyu huimarishwa kwa shughuli za hirimu mbali mbali za wazee na vijana ambao hutenda kwa umoja katika siasa, starehe, dini na uchumi katika kabila la Gikuyu.

 

 

 

Kutoka kitabu cha Jomo Kenyatta, Naushangilia Mlima wa Kenya.



Reference
362
Grammar
Vocabulary

Special Characters
Instructors Notes


© 2002 Rutgers University, excluding excerpted material that remains under the ownership of the existing copyright holders.

digiclass_help@brokenmail.rutgers.edu please replace "brokenmail" with ctaar.rutgers.edu