|
|
 |
Utangulizi
ugha yoyote, hasa
lugha iliyo hai na inayokua, inatokana na mazingira maalumu ya watu na utamaduni
wao. Kiswahili ni lugha ya Afrika Mashariki iliyoenea na kujulikana na wengi
zaidi katika Afrika Mashariki kuliko lugha nyengine yoyote ya Afrika. Kuna
wakati, na pengine mpaka leo, ambapo lugha hii ilikuwa ikiambiwa ati ni ya
kigeni, yaani asili yake si Afrika. Hivi leo ni wachache ambao wana mawazo hayo,
nao huwa
hawayatamki kwa
kuchelea kuthibitishiwa kuwa ni wajinga wa historia na mambo yalivyo. Maana
jambo hilo, kuwa Kiswahili ni
lugha ya kienyeji, limethibitishwa kabisa pasi na kubakisha chembe ya
shaka.
Wengine wameshikilia
kuwa utamaduni wa Kiswahili ni wa kigeni na kuwa hakuna kamwe watu hao waitwao
Waswahili. Kama ambavyo lugha ya
Kiswahili imethubutu kuwa ni lugha ya Afrika, utamaduni wake nao vile vile una
ithibati kamili kuwa ni utamaduni wa Afrika. Kama ambavyo Uhabashi
haukuwa utamaduni wa kigeni kwa kufungamana na Ukristo, na Uswahili pia
haukuwa utamaduni wa kigeni kwa kufungamana na Uislamu. Hali kadhalika Uswahili
haukuwa utamaduni wa Kiarabu kwa sababu hiyo hiyo. Utamaduni wa Kiswahili
chimbuko lake
ni mwambao wa Afrika
Mashariki. Ukichukua tawi lolote la mila na utamaduni wake utaona kuwa shina
lake
ni Afrika. Ukichukua
matanga ya Kiswahili, harusi, malezi,
itikadi, ukayalinganisha na ya Kiarabu, utaona kuwa ada zao ni tofauti. Kabila
nyengine zitokazo ng'ambo ya bahari ni vivyo hivyo.
Ukizifananisha ada za
Kiswahili na za kabila nyengine za kihuku utaona kuwa zimeelekeana, ingawa si
sawa sawa kabisa, maana ada hizo zitakuwa ni za kabila mbili tofauti. Tofauti
kama hiyo vile vile inaweza kupatikana kati ya kabila
mbalimbali za Kiswabili, ingawa kwa uchache sana. Tuchukue mfano wa
pepo. Waswahili wote wanazo itikadi za kupagawa na pepo au kuwa na pepo
kichwani. Wote wana uganga wao wa kumchomoa (kumkomoa), kama kumpigia kofi, na
kadhalika. Kabila mbalimbali za Kiswahili zitakuwa
na majina mengine mengine ya pepo na njia tofauti kidogo za kuwachomoa. Kabila
zisizokuwa za Kiswahili, ambazo ni jirani na Waswahili, zitakuwa pia
zimeambukizwa na itikadi hizo; lakini kabila nyingi za Kibantu itikadi zao ziko
kalika uchawi kuliko katika pepo.
Utamaduni wa
Kiswahili, mazingira yake hasa ni ile sehemu ya nchi iliyopakana na maji ya
pwani. Na huku Afrika Mashariki imesadifu kuwa mwambao mzima wenye urefu wa
kilomita kama 1500, na visiwa vyote
vilivyopakana na mwambao wenyewe vimekaliwa, mpaka hivi karibuni, na kabila za
Kiswahili. Nimesema mpaka hivi karibuni kwa sababu hivi sasa ziko sehemu
nyengine za mwambao wa Afrika Mashariki ambazo kabila nyengine, licha zile
zilizo jirani na Waswahili lakini hata nyengine ambazo zatoka masafa ya hata
kilomita 1500 bara, zimeshagota mpaka pwani. Lakini kwa kuwa
mazingira haya si asili yao, basi kazi, lugha na
utamaduni wafuatao ni wa Kiswahili, si wa asili ya kabila hizo. Basi utamaduni
wa mazingira ya Kiswahili una ngano zake na mengine ya fasihi-simulizi, una
lugha yake, una itikadi na sherehe zake, na juu ya yote una watu wake ambao
tokea kale—na kale hiyo haijulikani katika historia simulizi peke yake
bali pia katika historia za chimbo na historia za maandishi—mpaka leo
wanatambulikana ni wenye utamaduni huo, nao ni Waswahili.
Kama ambavyo watu ambao
asili yao ni bara hili la
Afrika waliitwa Waafrika, na kama ambavyo Waafrika
wengi wanaopatikana katika sehemu kubwa ya Afrika iliyo kusini ya jangwa la
Sahara wanatambulikana kuwa
ni Wabantu, basi Wabantu wa upwa wa Afrika Mashariki na visiwa mbalimbali vilivyo
jirani ni Waswahili; nao wana kabila zao maalumu mbalimbali, na ndani ya kabila
hizo muna magawanyiko ya vijikabila, na ndani ya vijikabila hivyo muna mbari na
koo.*
Huu ni utangulizi wa
historia ya Kiswahili, si historia ya Waswahili ambayo kuieleza kamili yahitaji
kitabu (au hata vitabu) kikubwa zaidi ya hiki. Basi naitoshe kueleza kwa uchache
hapa kuwa kabila za Kiswahili zilizoko pande mbalimbali, k.m. Wagunya,
Washaka, Wapaza, Wasiu, Wamvita,
Wakilindini, Wajomvu, Wabarawa, Washomvi, Wapemba, Watumbatu, Wamtang'ata,
Wangazija, n.k., zimeenea sehemu mbalimbali za mwambao wa Afrika
Mashariki na visiwa vyake.
Mambo muhimu yafaayo
kuyakumbuka kuhusu Waswahili ni kuwa:
(a) Kwa sababu ya
kukua kwa dola mbalimbali, Waswahili wamegawanyika na kuwamo katika nchi zaidi
ya tatu, na kwa sababu hiyo katika kila nchi idadi ya Waswahili imekuwa ni
chache. Vile vile, kwa sababu ya siasa, Waswahili hawakujitokeza mahali kwa jina
la Uswahili, bali huwa wamejitokeza kwa jina
la kabila, hasa katika sehemu ambazo hawa kuingiliwa na kabila nyengine,
kama Wagunya (Bajuni) na
Wangazija, n.k. Jambo hili, kwa upande mmoja, limekuwa ni la manufaa ingawa kwa
upande mwengine limekuwa ndiyo sababu ya kupingwa kuwepo kwao maana sauti
yao imekuwa ndogo.
Manufaa yake yamekuwa ya jumuiya pana zaidi kuliko Waswahili wenyewe; lugha
yao imefanya kazi ya
kuyaunga- nisha makabila ya Afrika Mashariki, matumizi ya lugha
yao yameenea
sana hata lugha ya
Kiswahili ikahitajiwa kuwa ndiyo lugha kubwa ya siasa wakati wa kupigania uhuru
na baada yake, na ndiyo kitambulisho cha dola mpya za
Tanzania na pengine
Kenya na
Uganda. Kwa sababu ya
mahitajio hayo ya kidola, imekuwa rahisi kukubali kuwa lugha ya Kiswahili ndiyo
lugha ya dola si kwa sababu ya kuenea kwake tu lakini pia kwa sababu
Waswahili wamekuwa ni watu ambao hawana sauti (ndipo hata wengine wakaweza
kusema kuwa Waswahili hawako kamwe). Basi kwa kuwa sauti ya Waswahili ni ndogo
na haisikiwi, ikawa hapana husuda za kikabila. Yaani, kabila nyengine za Afrika
Mashariki hazikupinga matumizi ya Kiswahili na kufanywa lugha ya taifa kwa kuwa
wenyewe Waswahili hawana njia
ya kunufaika zaidi ya wengine.
(b) Asili ya Waswahili
ni kuhesabu ukoo kukeni. Hili si jambo geni wala si la Waswahili peke
yao. Ziko kabila kadha wa
kadha za Kiafrika, nyengine zao ziko jirani na upwa wa Afrika Mashariki, ambazo
zinahesabu koo zao kukeni. Fahari ya Mswahili iko kwa mama wala si kwa baba.
Kabila namna hizi huwa hazipingi kuolewa na wageni, maana kuolewa na watu walio kando ya
kabila hilo huwa hakuathiri mila
yao wala kizazi chao kwa
sababu mtoto azaliwaye huwa si wa kabila ya mume wa kigeni bali ni wa kabila ya
Kiswahili. Tokea azali watukufu wa miji ya Waswahili, pepo wao, watukufu wao na
kadhalika, wamekuwa na majina ya kike—kina Mwana Chambi,
Mwana Mkisi, Mwana Mtwapa, Mwana Upatu, n.k.
Juu ya mpango huu
ukaingia mpango wa kuhesabu nasaba kuumeni, na hili limeingia zaidi kwa sababu
ya dini. Sasa basi, watu wa kabila nyengine waliozalikana na Waswahili, kwa
mfano Waarabu, huwa kwa upande mmoja wajihesabu kuwa ni Waswahili na upande
mwengine wanavutika upande wa kabila ya baba. Na hii ni sababu moja ya
kutowafahamu, au ya kutotaka kuwafahamu Waswahili ni nani. Utamaduni
upo,
lugha ipo lakini watu waambiwa hawapo kwa sababu tu ya kuwa wengine wanatiwa
katika nasaba nyengine zisizokuwa za Kiswahili—Waarabu, Wadigo, Wabondei, n.k.
Na ikiwa hapana budi kukubali kuwako kwao Waswahili, basi hukubaliwa lakini
wakatiwa ila ya kuwa si kabila safi, ni kabila ya
mchanganyiko. Hivyo ndivyo ilivyojaribiwa kufanywa hiyo lugha yenyewe, yaani
kuambiwa kuwa Kiswahili ni lugha ya kigeni hapa Afrika
Mashariki, ni lugha ambayo si safi, ni mchanganyiko wa
lugha. Haya kwa hakika si mambo ya miaka mingi sana. Kabla ya Afrika
Mashariki kutawaliwa na Waingereza hakukuwako na shaka yoyote juu ya kuwako kwa
kabila ya Waswahili, wala lugha yao, wala utamaduni wao.
Mbegu hizi za tuhuma juu ya Waswahili zilianza kupandwa wakati wa mamlaka ya
ukoloni wa Kiingereza, na zikashika nguvu zaidi wakati ambapo nchi za Afrika
Mashariki zinakaribia kuwa huru.
(c) Waswahili,
utamaduni wao na lugha yao, wako katika ukingo
wa Bara Afrika na Bahari ya Hindi. Bahari yenyewe imeumbika kwa namna ambayo
pepo zake na mikondo yake imezifanya safari za baina ya upwa wa Afrika Mashariki
na pwaa nyengme zilizoiambaa bahari hiyo kuwa ni za sahali
sana. Basi ikawezekana kwa
watu wa ng'ambo mbili hizi kuendeana ili kufanya biashara na kuingiliana
kitamaduni. Haya ni maingiliano ya pekee yaliyopata kutokea nyakati hizo baina
ya Waafrika na wageni wasio Waafrika. Tena ma-ingiliano haya yalianza kale zaidi
kuliko maingiliano ya baina ya Waswahili na Waafrika wenzao walioko kando ya
ukingo wenyewe kwani
maingiliano yao hayakuwako mpaka
baada ya Waafrika hao kujongea karibu zaidi na ukingo. Waafrika wa kwanza
walioanza kuwa na maingiliano ya namna hiyo na Waswahili walikuwa ni watu wa
kumbo la Kushiti, yaani Waboni, Wagala,
Wasomali, n.k. Baadaye ndipo wakawa na maingiliano na Wabantu wenzao,
kama vile Wapokomo
Wagiriama, Wadigo na
wengineo.
Katika maingiliano ya
kibinadamu, hapana budi watu hao kuathiriana, na haiwezekani athari zenyewe
zikawa ni za upande mmoja tu. Basi katika maingiliano ya Waswahili na watu
wengine, Waswahili—lugha yao na utamaduni
wao—hawakukosa kuathiriwa. Lakini athari hizo hazikuwabadilisha na kuwafanya
kuwa ni watu wengine bali wamebaki kuwa ni Waswahili vile vile. Na kwa upande
mwengine, wageni waliokuwa na maingiliano na Waswahili waliathirika zaidi na
Uswahili kuliko Waswahili walivyoathirika na athari za wageni hao. Maana
kumepatikana wageni ambao baada ya kuja pande hizi hawakurudi tena makwao,
wakazikukuta lugha zao na utamaduni wao na badili yake wakafuata utamaduni na
lugha ya Kiswahili. Na wale wageni waliojaaliwa kurudi makwao walirudi na athari
za Uswahili. Basi kwa upande huu, Uswahili umeuletea fahari Uafrika kwa
kuzieneza athari za Kiafrika nje ya bara hili.
Vile vile, yale madai
ya kuwa ustaarabu wa Uswahilini na miji yake imeamirishwa na kubuniwa na wageni,
yatokana na Wazungu. Maana hakuna hata mmoja kati ya wageni wa mwanzo mwanzo
waliokuja pande hizi—si Waarabu, si Wareno, si Wahindi, si Waajemi wala si
Machina—waliodai hivyo. Kwa
kuwa miji hii ilipata kukaliwa, na hata kutawaliwa, na Waarabu, Wareno, n.k.,
haiwi ni sababu ya kuifanya kuwa imebuniwa na wao. Kwani Wazungu pia waliikalia
na kuitawala miji hii, lakini hawawezi kudai kuwa wao ndio walioianzisha. Basi
na lugha ya Kiswahili ni vivyo hivyo; haikubuniwa na Waarabu wala na kabila
nyengine yoyote. Waarabu waliikuta lugha hii wakaipiga pambaja; na kwa
maingiliano ya utamaduni na utawala, maneno machache ya lugha
yao yakaingia katika
lugha hii ya Kiswahili—jambo ambalo lafanyika katika lugha
zote.
Nyakati zenda
zikibadilika. Hapo kale maingiliano ya Waswahili yalifungamana zaidi na upande
wa bahari. Lakini kila kukicha maingiliano hayo yalizidi kupungua na badili yake
yakaongezeka upande wa Bara Afrika. Hivi leo maingiliano ya lugha na utamaduni
yamefungamana zaidi na Uafrika na
kukata uhusiano wake na ng'ambo ya pili ya bahari.
Kabla ya kumaliza,
napenda kueleza kuwa kitabu hiki kinashughulika na historia ya lugha ya
Kiswahili wala hakikuingilia historia ya lugha mbalimbali za Kiswahili ingawa
zimedokezwa-dokezwa tu katika Sura ya Nne. Vile vile kitabu hiki hakikuingilia
historia ya fasihi ya Kiswahili, jambo ambalo pia ni muhimu katika mazungumzo ya
historia ya Kiswahili, isipokuvva kumetajwa baadhi ya ngano na mashairi kuwa ni
mifano tu zaidi ya kuwa ni maelezo ya historia zake.
Matarajio yangu ni
kuwa waandishi wengine wa historia watayafanyia uchunguzi zaidi mambo haya na
maenezi ya lugha ya Kiswahili, na hasa pingamizi zilizowekewa lugha hii na
ukoloni wa Kiingereza, ili watutolee vitabu muwafaka.
--------------------------------------------------
*Kadhalika tazama Shihabuddin Chiraghdin, 'Kiswahili na Wenyewe na
Kiswahili tokea Ubantu hadi Ki-standard', Mulika, na. 5, Septemba 1974
(Chuo cha Uchunguzi wa Lugha ya Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam).
HISTORIA YA
KISWAHILI,
Shihabuddin Chiraghdin
na Mathias Mnyampala
|
 |
| Reference |
 |
 |
|
|
 |